Mwanabaharia wa Umulkheir Said Abdi atangaza azma ya kuwania uongozi wa Mkomani
Na Mwandishi Taifa Leo news
Mjasiriamali na Mkurugenzi wa FASMU Freight Forwarding Limited, Umulkheir Said Abdi, ametangaza azma yake ya kuwania wadhifa wa Mwakilishi wa Wadi (MCA) wa Mkomani katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, akiahidi kuongoza ajenda ya maendeleo itakayoboresha maisha ya wakazi wa eneo hilo.
Bi Abdi alisema ameamua kuingia katika siasa baada ya kuona changamoto zinazowakabili wananchi wa Mkomani na kuamini kuwa uzoefu wake wa karibu miongo miwili katika uongozi wa biashara unaweza kutumika kuleta mabadiliko chanya katika utumishi wa umma.
"Nimefanikiwa katika biashara na sasa nataka kutumia uzoefu huo kuwatumikia wananchi. Dhamira yangu si kujinufaisha binafsi, bali kuhakikisha wanawake, vijana na watoto wa kike wanapata fursa za elimu, mafunzo ya ujuzi na kujitegemea kiuchumi," alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kampuni yake ya FASMU Freight Forwarding Limited, iliyoanzishwa mwaka 2006 na kupata leseni ya Mamlaka ya Ushuru Kenya (KRA) mwaka 2008, imejijengea jina katika sekta ya uondoaji na usafirishaji wa mizigo kupitia Bandari ya Mombasa hadi mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki, ikiwemo Sudan Kusini.
Akizungumzia Mkomani, Bi Abdi alisema wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za barabara mbovu, mifereji isiyotosheleza, mafuriko kila mvua inaponyesha, ukosefu wa taa za barabarani, huduma duni za afya, changamoto katika elimu na usalama.Alisema iwapo atachaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, atashirikiana na serikali ya kaunti, viongozi wengine na wadau mbalimbali kuhakikisha miundombinu inaboreshwa, mifereji ya maji inajengwa ili kudhibiti mafuriko, taa za barabarani zinaongezwa, na mazingira bora yanawekwa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.
Aidha, alisema ataweka mkazo katika kuwawezesha wanawake na vijana kupitia mafunzo ya ujasiriamali, upatikanaji wa mitaji, ukuzaji wa vipaji vya michezo na kuhimiza elimu kwa watoto wa kike.
"Nataka Mkomani iwe wadi yenye barabara bora, usalama wa kutosha, huduma bora za afya na elimu, pamoja na fursa za ajira kwa vijana. Hayo ndiyo maendeleo ninayotaka kuyaona ifikapo baada ya uchaguzi wa 2027," alisema.
Bi Abdi pia alisema ushiriki wake katika Kongamano la Women Achievers, ambapo alihudhuria kama Mratibu wa Kaunti ya Mombasa, umeimarisha azma yake ya kuhimiza wanawake kushiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi.Aliwahimiza wakazi wa Mkomani kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027 na kuwachagua viongozi kwa kuzingatia uwezo, uadilifu na maono ya maendeleo.
"Naamini uongozi ni huduma. Nikipewa nafasi na wananchi wa Mkomani mwaka 2027, nitafanya kazi kwa bidii, uwazi na ushirikiano ili kuhakikisha wadi yetu inapata maendeleo yanayostahili," alisema.
Comments
Post a Comment