Wadau Wakutana Nairobi Kuimarisha Sekta Nyama ya Nguruwe Huku Mahitaji Yakiongezeka
Na Kasuku David
taifaleo digital
Sekta ya nguruwe nchini Kenya inazidi kujitokeza kama nguzo muhimu ya uchumi wa kilimo, huku wadau wakisisitiza umuhimu wa uwekezaji wa kimkakati ili kunufaisha wakulima na kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya soko.
Katika mkutano uliofanyika katika Safari Park Hotel jijini Nairobi, ulioandaliwa na Farmer’s Choice Limited kwa kushirikiana na Shirika la uimarishi wa mifugo, ilibainika kuwa sekta hii tayari inasaidia zaidi ya kaya milioni 1.5.
Licha ya mchango wake wa takriban Shilingi bilioni 19.5 kwa uchumi wa mifugo, matumizi ya nyama ya nguruwe bado ni ya chini—yakikadiriwa kuwa kilo 0.4 kwa mtu kwa mwaka. Hii inaashiria pengo kubwa la uzalishaji, hasa wakati ambapo mahitaji yanatarajiwa kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 125 kufikia mwaka 2030.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Mifugo Jonathan Mueke alieleza kuwa serikali inalenga kuimarisha sekta hiyo kupitia sera bora, utafiti na huduma za ugani ili kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji.
Serikali pia imeahidi kuboresha miundombinu ya masoko, ikiwa ni pamoja na minyororo ya baridi na vituo vya uchakataji, ili kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya uhakika na bei nzuri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Farmer’s Choice Limited, Felisters Gitau Mutugu, alisisitiza haja ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ili kushughulikia changamoto kama gharama ya juu ya malisho, magonjwa ya mifugo na ukosefu wa masoko.
Mbali na faida za kiuchumi, sekta ya nguruwe ina mchango mkubwa katika lishe bora. Nyama ya nguruwe ina protini ya hali ya juu pamoja na vitamini muhimu kama B1, B6 na B12, pamoja na madini kama chuma na zinki. Aidha, nguruwe huzalishwa kwa muda mfupi na zina athari ndogo kwa mazingira ikilinganishwa na mifugo mingine.
Wadau wanaamini kuwa iwapo juhudi hizi zitatekelezwa ipasavyo, sekta ya nguruwe itakuwa suluhisho muhimu katika kupunguza uhaba wa protini, kuongeza kipato cha wakulima na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Comments
Post a Comment