RAIS RUTO AZINDUA MIUNDOMBINU KAUNTI YA TAITA-TAVETA: RELI YA VOI–MWATATE, BARABARA NA BANDARI KAVU KUPIGA JEKI BIASHARA


 Kasuku David – Taifaleo

Rais William Ruto  leo amezindua rasmi ukarabati na uboreshaji wa reli ya Meter Gauge Railway (MGR) ya Voi–Mwatate katika eneo la Mariwenyi, Kaunti ya Taita-Taveta, mradi mkubwa unaogharimu Shilingi bilioni 5.5 na unaotarajiwa kukamilika mapema mwaka ujao.
Mradi huo unalenga kufufua ukanda muhimu wa biashara wa Mombasa–Voi–Taveta–Moshi–Arusha–Singida–Bujumbura, ambapo utapunguza umbali kati ya Mombasa na Bujumbura kwa kilomita 358, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama za usafirishaji na kuimarisha biashara ya kikanda na kimataifa.

Aidha, mradi huo utajumuisha ujenzi wa bandari kavu (dry port) mjini Voi, ambayo itaifanya mji huo kuwa kitovu kikuu cha usafirishaji na biashara kinachounganisha Bandari ya Mombasa na mpaka wa Taveta/Holili One-Stop Border Post kati ya Kenya na Tanzania.
Katika hotuba yake, Rais Ruto alisema serikali yake imejikita katika kuharakisha miradi ya miundombinu kama njia ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi, akisisitiza kuwa maendeleo ya barabara, reli na mipaka ya biashara ni msingi wa mageuzi ya kiuchumi nchini.
Gavana wa Taita-Taveta Andrew Mwadime aliipongeza serikali ya kitaifa kwa kuleta miradi hiyo, akisema ni mabadiliko makubwa kwa mustakabali wa kaunti hiyo. Alieleza kuwa miradi ya reli na barabara itafungua ajira kwa vijana, kuongeza fursa za biashara, na kuinua sekta za kilimo, madini na utalii ambazo kwa muda mrefu zimekuwa nguzo kuu za uchumi wa eneo hilo. Mwadime aliongeza kuwa Taita-Taveta sasa inaelekea kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji na biashara ya mipakani katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Rais pia alikagua miradi kadhaa ya barabara ikiwemo Mto Mwagodi–Dawida–Mbale–Wundanyi–Bura Junction yenye urefu wa kilomita 55, pamoja na Illasit–Rombo–Njukini–Taveta yenye kilomita 60 ambayo imekamilika kwa asilimia 20.

Aidha, alieleza kuwa Cess–Lake Jipe inaendelea kujengwa, zabuni ya Maungu–Kasigau imetangazwa, na fedha za Voi–Sagalla zimehakikishwa. Serikali imesisitiza kuwa miradi hiyo inalenga kuimarisha mawasiliano, kuongeza biashara ya mipakani na kuleta mageuzi ya kiuchumi Taita-Taveta na maeneo jirani.


Comments

Popular posts from this blog

Patrick mucheleka calls for importance of turning restoration commitments into practical actions.

Kenya to Launch AI-Powered Disability Innovation Project at Kenya Institute of Special Education

Dr. Igbemi Arthur Igbemi: Health Sector Reformer Rising to Pan-African Recognition and Impact