MWANASIASA NA MWANA HARAKATI WA JAMII DANDORA AITAKA SERIKALI KUTUMIA ELIMU KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA
Mgombea ubunge wa Dandora North na mtaalamu wa elimu, Profesa Dorcas Mwigereri, ametoa wito kwa serikali kuhakikisha mpito wa asilimia 100 wa wanafunzi kutoka shule za msingi hadi sekondari kama njia bora ya kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu katika maeneo ya kipato cha chini.
Akizungumza katika Shule ya Sekondari ya Dandora wakati wa hafla ya kumpongeza mwanafunzi bora wa KCSE 2025, Bw. Aggrey Mnandi aliyepata alama ya A-, Profesa Mwigereri alisema elimu ndiyo nyenzo kuu ya kubadilisha maisha ya vijana na kuboresha taswira ya Dandora.
Alisema watoto wengi huingia katika matumizi ya dawa za kulevya kutokana na kukosa fursa za elimu unaosababishwa na umasikini. Alitoa wito kwa serikali chini ya uongozi wa Rais William Ruto kuweka elimu kama kipaumbele cha kitaifa, akionya kuwa kuwaacha watoto nje ya shule ni kuhatarisha usalama wa jamii kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Dandora, Bw. Thiong'o alimpongeza mwanafunzi huyo kwa bidii, nidhamu na juhudi zake, akisema mafanikio hayo ni ushahidi kuwa vijana wa Dandora wana uwezo mkubwa endapo watapewa mazingira bora ya kujifunzia. Aliwataka wadau wa elimu na serikali kuongeza ufadhili kwa shule za maeneo ya kipato cha chini ili kuhakikisha wanafunzi wote wanakamilisha masomo yao bila vikwazo.Hon Mwigereri aliahidi kuifanya elimu, uwezeshaji wa vijana na wanawake kuwa nguzo kuu ya ajenda yake ya uongozi iwapo atachaguliwa kuwa mbunge wa Dandora North.
Comments
Post a Comment